Lipumba- Cheo cha Naibu Waziri Mkuu Hakipo Kikatiba

Mwenyekiti wa Chama Cha CUF Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na Clouds Tv ametoa maoni kuhusu uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Naibu Waziri Mkuu. Profesa Lipumba ametoa historia ya jinsi utaratibu huo ulivyoanzishwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Kwa mujibu wa Lipumba, Rais Mwinyi alianzisha utaratibu huo kwa kumteua Salim Ahmed Salim kuwa Naibu Waziri Mkuu. Salim Ahmed Salim alikuwa Waziri Mkuu hapo awali, na kwa mujibu wa taratibu na katiba, alipochaguliwa kuwa Rais, naibu wa kwanza wa Rais alitoka Tanzania Bara. Pia, Rais Mwinyi aliamua kumteua Marehemu Mrema kuwa Naibu Waziri Mkuu.

Profesa Lipumba ameashiria kwamba katiba ya sasa ya nchi inaeleza wazi cheo cha Waziri Mkuu, lakini hakijaeleza kwa kina kuhusu cheo cha Naibu Waziri Mkuu. Hata hivyo, ameeleza kuwa Rais ana mamlaka ya kuunda Wizara na kuteua viongozi, ikiwa ni pamoja na kuteua Naibu Waziri Mkuu. Profesa Lipumba ameongeza kuwa labda Rais amefanya uteuzi huu kutokana na hitaji la Waziri Mkuu kupata msaada zaidi katika majukumu yake, na hivyo kuamua kufanya uteuzi huo.

Kwa maneno yake, “Uteuzi huu wa Naibu Waziri Mkuu unaweza kuwa sehemu ya jitihada za kuboresha utendaji wa serikali, kwa kuwa Waziri Mkuu anaweza kuhitaji msaidizi wake katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku,” alisema Profesa Lipumba, Mwenyekiti wa Chama Cha CUF.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *