Taarifa mbaya kwa mashabiki wa Stars, Simba kuhusu Kapombe

Beki wa kikosi cha awali cha Taifa Stars kinachotarajiwa kwenda nchini Misri katika michuano ya AFCON 2019 Shomari Kapombe ameumia akiwa kwenye kikosi hicho kilichoanza mazoezi yake jana kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa beki huyo wa Simba baada ya kuwa nje ya dimba kwa zaidi ya miezi saba akiuguza majareha aliyoyapata mwezi Novemba mwaka jana nchini Afrika Kusini alipokuwa na kikosi cha timu ya taifa kilichokuwa kikijiandaa na mchezo wa kufuzu AFCON dhidi ya Lesotho.

Kocha Emmanuel Amunike aliamua kumjumuisha katika kikosi hicho cha awali kilichotangaza mwezi Mei mwaka huu, baada ya mchezaji huyo kupona majeraha yake na kuanza mazoezi tayari kwa kurudi dimbani licha ya klabu yake ya Simba kutomtumia katika mechi za mwisho za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Leo Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo amethibitisha kuwa mchezaji huyo amejitonesha majeraha hayo wakati akiendelea na mazoezi katika kambi ya Taifa Stars iliyoanza rasmi Juni 01, 2019 kwenye Hoteli ya White Sands hivyo kwa sasa anasubiri hatma yake kwenye kikosi cha mwisho kitakachotajwa hivi karibuni.

“Shomari Kapombe amejitonesha wakati akiendelea na programu ya timu ya taifa hivyo kwasasa hayuko na wenzake lakini anaendelea kufuatilia programu ya mazoezi mpaka hapo mwalimu atakapotaja kikosi cha mwisho”, amesema Ndimbo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *