Wabunge wachangia Sh milioni 32 kwa mwanamke aliyejifungua mapacha wanne

Wabunge  wamechanga zaidi ya Sh.Milioni 32, kwa ajili ya mwanamke Radhia Solomon ambaye alijifungua mapacha wanne katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambapo alikimbiwa na mumewe.

Fedha hizo zimetokana na wabunge wanaume 248 kukatwa Sh.100,000 huku wanawake 145 wakikatwa Sh.50,000 na kupata kiasi cha Sh.32,050,000.

Mama huyo alitinga jana bungeni akiwa na watoto wake akisaidiwa na mama yake mzazi, mama yake mkubwa na Afisa ustawi wa jamii.

Akitambulisha wageni baada ya kipindi cha maswali na majibu, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtambulisha Radhia na kudai kuwa baada ya kujifungua mume wake alimkimbia kuwajibika.

“Naomba nimtambulishe kwenu Radhia Solomon ambaye alijifungua watoto wanne kwa uzazi mmoja lakini bahati mbaya mwanaume wake alikimbia majukumu, baada ya kupata watoto wanne ilimhitaji kupata usaidizi na kutokana na maisha ya Dar es salaam ni ngumu kidogo,”alisema.

Ndugai alisema mama huyo anasaidiwa kulea watoto na mama yake mzazi, mama yake mkubwa na Afisa ustawi wa jamii.

“Kwa hiyo ndugu zangu amekuja hapa ili sisi kama Bunge tukemee wanaume ambao hawawajibiki lakini pia kama kawaida tumsaidie,”alisema.

Kabla ya kufikia muafaka wa kumchangia, Mbunge wa Viti maalum (CUF), Rukia Ahmed Kassim alisema kwasababu wanaume wamezoea kutelekeza watoto anapendekeza wabunge wanawake wachangie Sh.50,000 na wanaume wachangie Sh.100,000, hoja iliyoungwa mkono na Mbunge wa Viti maalum(Chadema), Susan Lyimo.

Hata hivyo, Mbunge wa Geita vijijini(CCM), Joseph Musukuma alipendekeza wabunge wakatwe posho ya siku nzima ili wamsaidie mama huyo.

Akihitimisha hoja, Spika Ndugai alisema wabunge wamekubaliana kuchanga fedha hizo ambapo wabunge wanawake watatoa Sh.50,000 huku wanaume Sh.100,000.

Januari 8, mwaka huu Radhia alijifungua pacha wanne katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *