Diamond amwaga sifa kwa Harmonize, atoa ushauri kwa wasanii wenzake

Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Harmonize, kutoka WCB, jana Alhamisi, Mei 23, 2019 aliandaa hafla ya kufuturisha katika Ukumbi wa Serena Hotel ambapo pia aliutambulisha wimbo wake wa ‘Never Give Up’

Hafla hiyo ilihudhuriwa na mastaa wenzake wakiwemo wasanii wote wa WCB wakiongozwa na Diamond Platnumz, lakini pia viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, Katibu Mkuu wa Basata, Godfrey Mngereza, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na wengine kadha wa kadha.

Kwa kutambua umuhimu wa Diamond ambaye kimsingi ndiyo bosi wake, Harmonize alimwalika kwenye kipaza sauti ili azungumze machache kuelekea uzinduzi wa wimbo huo.

Akizungumza baada ya kupewa fursa hiyo, Diamond amesema Harmonize ni msanii anamfanya ajivunie na kutembea kifua mbele.
Amesisitiza wasanii kushikamana kwa pamoja ili kupeleka Sanaa mbele kwani kwa sasa sanaa ni biashara na kuongeza kuwa si vyema kuona wasanii wakiishi kwa chuki na ugomvi baina yao.

Amesema anamshukuru Mungu kwa kuanzisha Lebo ya Muziki (Record Lebel) kwani kumewapa fursa wasanii kadhaa kupata fursa ya kujiongezea kipato.

“Faraja yetu ni kuwapa Watanzania wenzetu sifa na heshima, faraja yetu ni kuifanya Sanaa yetu kuheshimika na kuwapa ari vijana kuona kwamba kila kitu kinawezekana, hivyo tujitume na kumuomba sana Mwenyezi Mungu ili sote tuweze kufanikiwa,” amesema Diamond Plutnumz.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *