Muhimbili Yakamata Madaktari Feki

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imekamata madaktari feki wawili waliokua wakiwalaghai wagonjwa na ndugu zao kujipatia fedha isiyo halali.

Taarifa iliyotolewa jana Februari 28 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano, Neema Mwangomo imewataja madaktari hao feki kuwa ni Josephat Joseph na Khamis Hamid Bakari.

Kufuatia taarifa za wagonjwa na ndugu kuhusu madaktari hao feki, uongozi wa hospitali uliweka mtego na kufanikiwa kumkamata Josephat mnamo tarehe 27 Februari katika Kliniki ya magonjwa ya ngozi huku mshirika wake Khamis akikamatwa maeneo ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI)

Madaktari hao feki wamefikishwa kituo kikuu cha kati Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya hatua za kisheria.

Kufuatia hayo, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili umewataka wananchi kuchukua tahadhari na pia watumishi wake wote kuvaa vitambulisho muda wote wa kazi ili jamii iweze kuwatambua.

Aidha, Muhimbili imewakumbusha wananchi kuwa malipo yote yanafanyika kupitia kumbukumbu namba (Control namber) ambapo ukilipia jina la hospitali litatokea.

Nao wananchi wameombwa kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitali pindi wanapomtilia shaka mtoa huduma ili hatua iweze kuchukuliwa kuepuka madhara yanayoweza jitokeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *