Zitto Aendelea Kuwa Sahihi Aliyoyaibua Enzi za Magufuli

Kiongozi wa ACT Wazalendo na chama chake wamepokea sifa kutokana na kuwa sahihi katika kuibua na kukosoa mambo  mbali mbali ya kiuendeshaji Serikalini.

Mnamo April 11, 2019, Zitto akiichambua ripoti ya CAG wakati huo chini ya utawala wa Hayati Rais Magufuli alikosoa mfumo uliokua unatumiwa na Serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka wa watu kukiri makosa na kulipa fedha ‘Plea Bargain’.

Zitto kupitia ukurasa wake wa Twitter 2019 aliandika kuwa watamkumbusha CAG akague mapato yanayotokana na kubambikia watu kesi ili mwisho wa siku watoe pesa.

Zitto aliongeza kuwa utakatishaji fedha limekua shtaka la kuumiza watu, kukomoa na kupora mali za watu.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa bungeni Aprili, 2021 iliainisha kuwepo kwa fedha zaidi ya Sh50 bilioni zilizotokana na mali zilizotaifishwa na kurejeshwa serikalini chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP) hadi kufikia Juni 30, 2020 kupitia kesi zilizomalizika kwa kipindi cha miaka sita.

Oktoba 14, 2022, CAG Charles Kichere alisema ifikapo Machi, 2023 watamkabidhi Rais Samia ripoti ya matumizi ya fedha hizo zilizotokana na makubaliano ya washtakiwa na DPP.

Jambo lililoibua hisia kuwa Zitto alikua sahihi ni baada ya Jana Januari 31 Rais Samia kufunguka kuwa mfumo wa haki jinai nchini umevurugika na kufafanua kuwa katika Tume ya Taifa ya Mashtaka kulikuwa kuna ngoma kubwa kidogo inachezwa mpaka kufikia kukusanya fedha za adhabu ya makubaliano baada ya kukiri kosa.

Rais Samia alifafanua kuwa fedha hizo za plea bargain nyingine zimeonekana na nyingine hazijaonekana na uki-trace utaambiwa kuna akaunti China sijui imepeleka pesa zipi.

Kutokana na hayo Rais Samia jana aliunda Tume inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande, ambayo itakuwa na jukumu kubwa la kufanya maboresho ya haki jinai ili kukidhi matakwa ya serikali na jamii ya Tanzania kwa ujumla.

Rais Samia ameitaka tume hiyo kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini, kuchunguza suala hilo kwa kina na kutazama Ofisi ya Mashataka kuna nini.

Baada ya kuenea kwa habari hiyo kutoka kwa Rais Samia, Zitto alitumia ukurasa wake wa Twitter kumuomba Rais Samia kuweka wazi  kwa umma ukaguzi maalum uliofanywa na CAG utakaowasilishwa Tarehe 31 Machi mwaka huu.

Zitto alifafanua kuwa, lengo ni Watanzania wajue ukweli wa uporaji wa mali za watu uliofanyika na kuongeza kuwa ni muhimu waliodhulumiwa kufidiwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *