Wanaharakati Watishia Kulala nje ya Ikulu Serikali isipotimiza Matakwa Yao

Moses Kamau and Isaac Kamau from Haki na Ukweli in Nairobi on August 29, 2019

Wanaharakati wamemsihi DPP Noordin Haji kuhakikisha wote waliotajwa katika kashfa za ufisadi wanakamatwa bila mapendeleo. Wametishia kukita kambi kwenye lango la ikulu au Bunge serikali ikijitia hamnazo na kupuuza matakwa yao.

Haki na Ukweli, Shirika lisilo la Serikali, lilimesisitiza kuwa wengi ambao wametajwa katika kashfa kadhaa za ufisadi nchini wanaendelea kushikilia nyadhifa na hawajawahi kukamatwa.

Akiongea jijini Nairobi, Moses Kamau, afisa wa Haki na Ukweli, alisema hata ingawa kukamatwa kunatekelezwa, hakuna kesi ambayo imewahi kumalizika wala haki kutendeka.

“Tunafahamu fika kwamba licha ya watu wengi mashuhuri  kufikishwa mahakamani kutokana na ufisadi, wanaachiliwa na dhamana ndogo sana,” Kamau alisema. Kamau alisema kanuni za dhamana zimeshindwa kumaliza suala la ufisadi ambalo limekuwa mithili ya saratani nchini.

Karibia watu 1,000 wameshtakiwa mahakamani kwa sababu ya ufisadi tangu Rais Uhuru Kenyatta kuchukua madaraka mnamo 2013.

“Kila mtu ana machungu na serikali hii, tunataka wale waliohusika na ufisadi kupigwa marufuku ya maisha kushikilia wadhifa wowote,” Kamau alisema.

Wanaharakati wanasema licha ya kuwaandikia Mahakama, Bunge na EACC, bado hawajapata mawasiliano yoyote rasmi kuhusu hatma ya matakwa yao.

“Iwapo wao (Mahakama, Bunge na EACC) hawatuchukulia jambo hili kwa uzito, hatua itakayofuatia itakuwa kulala nje ya Ikulu au Bunge hadi matakwa yetu yatimie,” Maurice Masika alisema.

Ushindani wa Kenya kimataifa unazuiwa na ufisadi uliokita mizizi katika nyanja mbalimbali za uchumi.

Mapema wiki hii, Rais Uhuru Kenyatta aliwatia wafanyikazi wa Mamlaka ya Bandari za Kenya katika kurunzi kutokana na ufisadi. Alitishia kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana ya kashfa ya Kituo cha Mafuta cha Kipevu. Pesa karibia bilioni 40 zimenahofiwa kupondwa na maafisa wale.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *