Tarehe ya Uchaguzi wa Eneo Bunge la Kibra yatangazwa, Pata Maelezo kwa Kina…

IEBC Chairman Wafula Chebukati

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza Novemba 7 kama tarehe ya uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Kibra.

Hii inakuja baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kutangaza nafasi ya kiti hicho kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa Kibra Ken Okoth. Muturi alikuwa amemwandikia Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati mnamo Agosti 14 akimtaka afanye uchaguzi mdogo katika eneo hilo.

Tume hiyo inavitaka vyama vya siasa vinavyolenga kushiriki katika uchaguzi huo kupitisha majina ya wagombeaji wake wa kwanza mnamo au kabla ya Agosti 26.

“Afisa yeyote wa umma anayetaka kuwania nafasi hiyo anahitajika kujiuzulu katika nafasi yake  siku saba baada ya kutangazwa kwa nafasi hiyo,” Chebukati alisema katika Ilani ya Gazeti.

Image result for ken okoth

IEBC imesema mtu yeyote anayetaka kugombea kiti hicho kama Mgombea huru anatakiwa awe hajakuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa angalau miezi mitatu kabla ya uchaguzi mdogo.

Aidha, IEBC pia imesema vyama vya siasa vinavyotaka kuwasilisha wagombea wao katika uchaguzi sharti viwasilishe jina la mgombea ifikapo Septemba 3 baada ya kutatuliwa kwa chaguzi yote ya chama.

Kipindi cha kampeni ya uchaguzi huo kinatarajiwa kuanza Jumatatu, Septemba 9 hadi Jumatatu, Novemba 4.

Uchaguzi mdogo wa Kibra unakuja baada ya kifo cha Ken Okoth ambaye alifariki kutokana na saratani mnamo Julai 26 alipokuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Nairobi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *