MAHAKAMA KUU KUTOA UAMUZI WA KUSITISHA AMA LA KUAPISHWA KWA MBUNGE WA SINGIDA MASHARIKI AGOSTI 23

Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kusitisha ama la  kuapishwa kwa mbunge wa Singida Mashariki Agosti 23

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashatiki (Chadema), Tundu Lissu ameiomba Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya hati ya dharura itoe amri ya kusitisha mchakato wa kuapishwa kwa mbunge mteule wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM).

Maombi ya Lissu namba 18 ya mwaka 2019 yametajwa jana mahakamani hapo mbele ya Jaji Sirilius Matupa ambapo Lissu anawakilishwa na jopo la Mawakili wanne akiwemo Peter Kibatala, huku upande wa Serikali ambao ni wajibu maombi ukiwakilishwa na mawakili wanne akiwemo Wakili wa Serikali Mkuu, Vincent Tango.

Hata hivyo mahakama hiyo imepanga Agosti 23 mwaka huu kusikiliza maombi hayo ya Lissu ya kutaka Mbunge huyo Mtaturu asiapishwe Bungeni pamoja na maombi yake mengine ya msingi.

Katika maombi hayo mengine ya Msingi ambayo yaliwasilishwa na Wakili Kibatala Lissu anaiomba Mahakama kumwamuru Spika wa Bunge Job Ndugai awasilishe mahakamani taarifa ya kumvua Ubunge aliyoitoa bungeni ili iweze kupitia na kisha iamuru kuutengua na kuutupilia mbali.

Pia anaomba Mahakama imwamuru Spika ampatie yeye Lissu nakala ya taarifa ya kumvua ubunge.

Wakati akiwasilisha ombi la kuitaka mahakama itoe amri ya kusitisha kuapishwa kwa mbunge mteule Mataturu, Wakili wa Lissu ambaye ni Kibatala aliomba mwongozo wa mahakama ili waweze kuzungumzia suala hilo la kusimamishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, lakini ombi hilo likapingwa na mawakili wa Serikali wakidai kuwa kwa sasa sio muda sahihi wa kuanza kulisikiliza jambo hilo.

Pia upande wa wajibu maombi waliomba muda wa siku nane ili waweze kuwasilisha hati ya kiapo kinzani pamoja na hati ya maelezo kinzani kabla ya maombi hayo kupangiwa siku ya kuanza kusikilizwa.

Wakili wa Serikali Mkuu, Tango alisema wanaomba siku hizo kwa kuwa shauri hilo linahusisha mhimili mwingine, yaani Bunge hivyo wanahitaji kupata muda wa kushauriana na Bunge (Spika) ili kuweza kuandaa kiapo kinzani.

Hata hivyo Kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Kibatala alisema kuwa hana tatizo na wajibu maombi kuomba muda wa kuwasilisha hati ya kiapo kinzani lakini alisema kuwa muda wa siku nane walioomba ni mrefu sana kulingana na mazingira ya kesi hiyo wanaomba isikilizwe na kuamriwa ndani ya siku 14.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Sirilius Matyupa alisema atatoa uamuzi wa kusitisha mchakato wa kuapishwa kwa mbunge huyo mteule Mtaturu baada ya kusikiliza maombi yote ya Lissu, Agosti 23, mwaka huu.

Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku akisema kuwa si yeye aliyemvua ubunge Lissu bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.

Miongoni mwa sababu alizozitaja za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *