Matokeo Kidato cha tano: Kuripoti ndani ya siku 14 tu

Kufuatia orodha ya wanafunzi waliochaguliwa  kujiunga kidato cha tano mwaka 2019 nchini Tanzania ambapo muhula wa kwanza wa masomo unatarajiwa kuanza tarehe 8 mwezi julai mwaka huu, wanafunzi wote  waliopangwa  wametakiwa kuripoti katika shule husika ndani ya siku 14 kuanzia tarehe 8 julai.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo mjini Dodoma wakati akitangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi kwa mwaka wa masomo utakao anza mapema mwezi Julai, 2019.

Waziri Jafo amesema kuwa, endapo mwanafunzi atashindwa kuripoti ndani ya siku 14, nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi.

Katika hatua nyingine amesema, mabadiliko ya shule yataruhusiwa baada ya kumalizika muhula wa kwanza na zoezi hilo litazingatia uwepo wa nafasi kwenye shule kwa idhini ya afisa elimu wa mkoa husika.

“Nasema hivi kwa sababu, wakati mwingine tunatangaza matokeo, na mtu anataka palepale apate uhamisho, hilo jambo halitaruhusiwa mwaka huu. Hivyo muhula utakapokwisha, na ikithibitika kama ni kweli kuna haja mtu huyo ahame basi jambo ilo litaruhusiwa, lakini jambo hilo litaratibiwa na Maafisa Elimu Mikoa baada ya kuona kuna nafasi katika mkoa na shule husika ”

Waziri Jafo, amewatoa hofu wanafunzi waliofaulu na kukosa nafasi ambao ni jumla ya wavulana 1,861 kati ya wote waliochaguliwa ambao ni laki 110,555 na kuwataka wawe na subira kwani watachaguliwa katika awamu ya pili (Second selection). Aidha, wanafunzi wote wa kike waliofaulu, wamepata nafasi

Akitoa takwimu za ufaulu wa watahiniwa wa kidato cha Nne kwa mwaka 2018, kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu, alisema ni watahiniwa 113,825 kati yao wasichana ni 47, 779 na wavulana 66,046 sawa na asilimia 31.76 ya watahiniwa wote waliofanya mtihani

Mbali na hayo, Waziri Jafo  amewapongeza na kuwahimiza wanafunzi wote waliojiunga kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi wasome kwa bidii ili waweze kujiunga na elimu ya juu baada ya kufanya vizuri kidato cha sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *