Samatta:Kama Simba hawanitaki nitaangalia sehemu nyingine

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga kunako klabu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji, Mbwana Samatta, amesema kuwa endapo atamaliza harakati za maisha yake ya soka atarejea Tanzania kukipiga kunako klabu ya Simba.

Samatta amesema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na Azam TV wakati wa hafla ya ugawaji tuzo za ‘Simba Mo Awards’ ambapo ameweka wazi kuwa iwapo akitaka kurejea na wakamkubalia basi atakuwa tayari.

“Wachezaji wengi wakubwa wanapokaribia kustaafu soka hurudi kwenye vilabu vyao vya zamani ambavyo viliwatoa,” amesema Samatta.

“Nilikuwa mchezaji wa Simba zamani, hata nitakaporudi baadaye nafikiri nafasi ya kwanza itakuwa kwa Simba kwa sababu niliwahi kuitumikia lakini kama watakuwa hawanitaki ndio nitaangalia sehemu nyingine.”
.
“Kwa heshima yao kwa sababu niliwahi kuwa mchezaji wao kwa hiyo nafasi ya kwanza lazima itakuwa kwao.”

Samatta amewahi kuwa mchezaji wa Simba ambapo baadaye alikwenda TP Mazembe ambao walimsafishia njia na kujiunga na klabu yake sasa KRC Genk ya nchini Ubelgiji.

TP Mazembe walimuona Samatta wakati walipokuja kucheza na Simba mechi duru la pili katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika April 3, mwaka 2011 katika Uwanja wa Taifa ambapo Samatta alionesha kiwango bora sana akiwa ameingia kutoka benchi.

Katika mchezo huo Simba walifungwa mabao 2-3, huku Samatta akifunga goli moja.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *