Nyalandu ashangaa silaha kutumika kumkamata

Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, asilimulia jinsi walivyokamatwa na watu wenye silaha kama wao ni wahalifu jambo ambalo linasikitisha.

Nyalandu alieleza hayo leo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo alianza kuwashukuu wale wote walioguswa na mkasa uliompata Mei 27 mwaka huu huku akilifananisha tukio hilo ni sawa na kujaribiwa kwake.

Alieleza kuwa waliwasili katika kijiji cha Itaja wilayani Singida kuongea na viongozi wa vijiji na viongozi wa vitongoji kata ya Itaja kuhusu zoezi linaloendelea nchi nzima kwa ajili ya kuwatambua na kuwaandikisha wanachama.

“Kama ilivyoripotiwa kikao chetu cha ndani kilivamiwa na watu ambao hatukuwafahamu walikuwa na silaha na kuniamrisha pamoja na wenzangu wawili mwenyekiti wa Chadema kata ya Itaja na ndugu Peter tuondoke nao,”alieleza

Aliendelea kueleza katika ukurasa huo kuwa:”Sote tulipatwa na mshtuko mkubwa na hatukupewa utambulisho wala sababu ya kutolewa kwenye kikao na kuchukuliwa na watu wenye silaha mithili ya wahalifu, wote tulipigwa bumbuwazi la sitofahamu,”

Alisema walivyofika kila mmoja waliwekwa katika chumba tofauti na kuhojiwa juu ya uhalali wa kikao cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kudai kuwa kulikuwa na harufu ya rushwa.

Baada ya mahojiano, Nyalandu alisema walipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Singida na muda mfupi wakasikia Takukuru Singida wamejiridhisha hapakuwa na tatizo na kuwapeleka polisi.

“Polisi walitufanyia mahojiano mengine kwa kila mmoja wetu katika chumba tofauti na kutujulisha kuwa wao hawakuwa na neno lolote juu yetu, isipokuwa tukifanya kikao chochote wanataka tutoe taarifa kwa Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD) Singida na wamesema tupatiwe dhamana ili turudi Jumanne na kuripoti polisi na Takukuru endapo Takukuru watakuwa na neno.

Alieleza baada ya kupatiwa dhamana usiku huo ilitolewa amri kwamba wafutiwe dhamana na kulala kituoni hapo hadi Mei 28 mwaka huu walipopatiwa dhamana.

Takukuru mkoani Singida ilimkamata Nyalandu Mei 27 mwaka huu na wenzake wawili wakiwa katika kikao cha ndani ya chama kwa tuhuma za kuhusishwa na masuala ya rushwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *