Kauli mpya ya Makamba kuhusu mifuko ya plastiki

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira January Makamba amesema, watu wapatao 600 kutoka Baraza la Mazingira la taifa (NEMC) kwa kushirikiana na watu wa Serikali za Mitaa wanatarajiwa kuzunguka katika masoko na maeneo mengine nchi nzima kutoa elimu kuhusu katazo la mifuko ya plastiki.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ifikapo tarehe moja mwezi wa sita hakuna mwananchi yeyote atakayeruhusiwa kuonekana na mifuko ya plastiki nchini Tanzania.

Makamba ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii waTwitter kuhusu kutolewa kwa elimu hiyo na kuongeza kuwa, kwa mkoa wa Dar es salaam vigari 30 vimeandaliwa kupita mtaa hadi mtaa katika elimu kuhusu katazo hilo.

Kwa kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira serikali ya Tanzania imetunga kanuni za mwaka 2019 za kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.

Ambapo kifungu cha nane cha kanuni hizo kinaorodhesha makosa matano ambayo ni; kuzalisha na kuagiza mifuko ya plastiki, kusafirisha nje ya nchi mifuko ya plastiki, kuhifadhi na kusambaza mifuko ya plastiki, kuuza mifuko ya plastiki na mwisho kumiliki na kutumia mifuko ya plastiki.

Kwa kosa la uzalishaji na uagizaji adhabu yake ni faini isiyopungua TSh milioni 5 na isiyozidi TSh milioni 20, kifungo kisichozidi miaka miwili jela au kupewa adhabu zote mbili.

Kosa la kusafirisha mifuko nje ya Tanzania ni sawa na za kosa la uzalishaji hivyo adhabu zake kufanana huku  kosa la kuhifadhi na kusambaza mifuko likiwa na adhabu ya faini isiyopungua TSh milioni 5 na isiyozidi TSh miioni 52, kifungo kisichozidi miaka miwili au faini na kifungo kwa pamoja.

Ukipatikana na hatia ya kuuza mifuko ya plastiki adhabu ambazo utakumbana nazo ni pamoja na faini isiyopungua TSh laki moja na isiyozidi laki tano, pili, kifungo kisichozidi miezi mitatu jela au kupata adhabu ya faini na kifungo kwa pamoja.

Ukiwa mtu ataendelea kutumia na kumiliki mifuko ya plastiki kuanzia Juni 1 nchini Tanzania, basi atalipa faini isiyopungua TSh elfu 30 na isiyozidi laki mbili, kifungo kisichozidi siku saba ama faini na kifungo.

Mifuko ya plastiki ilikatazwa rasmi Tanzania aprili 9, 2019  kupitia kauli ya Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa,  Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *