Nyota hawa wa Yanga hatima yao haijulikani

Amissi Tambwe

Ni mchezaji ambaye misimu miwili nyuma alikuwa akifanya vizuri sana, amewahi kuibuka mfungaji bora tangu wakati akiwa Simba na Yanga pia. Amekuwa hatari sana mbele ya lango la timu pinzani akiwa katika ubora wake. Tangu msimu uliopita, Tambwe amekuwa hana wakati mzuri sana kutokana na kutopata nafasi kubwa ya kucheza kufuatia kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, umri pia umeanza kumtupa. Bado kocha Mwinyi Zahera anakuna kichwa kama ambakishe au aachane naye hasa kutokana na Mrundi huyo kumsaidia katika nyakati Fulani ngumu.

Thaban Kamusoko

Mzimbabwe huyo alijiunga na Yanga mwaka 2015 akitokea Zimbabwe. Alitokea kuwa moja ya viungo bora sana katika Ligi Kuu Soka Tanzania Bara. Amecheza Yanga kwa mafanikio makubwa akibeba ubingwa TPL mara mbili na Kombe la Azam Sports Federations Cup. Takribani miwili miwili amekuwa hayupo kwenye kiwango bora kutokana na kuandamwa na majeraha na hivyo kukosa nafasi ya kutosha. Mkataba wake na Yanga umeisha na anasubiri mustakabali wake kutoka kwa kocha wake licha ya kuonekana kuaga mashabiki kupitia Instagram yake.

 

Ibrahim Ajibu

Alijiunga na Yanga msimu wa 2017/2018 akitokea Simba akiwa na kiwango bora kabisa. Amecheza Yanga kwa misimu miwili yenye mafanikio makubwa kwa upande wake licha ya kutofanikiwa kuvuna hata taji moja. Amekuwa akiisaidia Yanga kwenye matukio tofautii tofauti. Hufunga magoli ya aina mbalimbali kama mipira ya adhabu na vile vile kutoa pasi murua za magoli. Tayari amemaliza mkataba wake na Yanga na anahusishwa kujiunga na Simba baada ya dili lake na TP Mazembe kubuma. Haijawekwa wazi kama atasalia hapo ama la!

Haruna Moshi

Ni moja ya viungo ambao wamewahi kutamba sana hapa nchini hususan wakati akicheza na klabu ya Simba. Alijiunga na Yanga mwishoni mwa mwaka jana kwa mkataba wa miezi sita. Tangu atue Yanga hajawa na kiwango bora pengine kutokana na umri kumtupa mkono. Mpaka sasa haijajulikana wazi kama ataendelea kubaki au safari yake kwa Yanga ndyo imeishia hapo.

Mrisho Ngassa

Amewahi kutamba sana miaka ya nyuma, ni moja ya wachezaji ambao walitokea kuwa kipenzi kikubwa cha WanaYanga kutokana na mapenzi makubwa kwa klabu hiyo na moyo wake wa kujitoa. Tangu asajiliwe Yanga amekuwa hana makali kama yale ya zamani, mkataba wake unaelekea ukingoni nab ado haijajulikana kama ataendelea kubaki au vinginevyo.

Ramadhani Kabwili

Mlinda mlango namba moja wa Yanga amekuwa bora msimu huu licha ya kutopewa nafasi mara kwa mara, kesho mkataba wake unakamilika licha ya awali kuelezwa kuwa alisajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano. Mpaka sasa bado hajazungumza na uongozi wa Yanga juu ya hatma yake, mbivu na mbichi zitajulikana kwani anafuatiliwa na timu moja iliyopo Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *