Ujenzi wa reli ya kati umefikia asilimia 47

 

Serikali imesema ujenzi wa reli ya kati ya kisasa (SGR) awamu ya kwanza kutoka Dar es salaam hadi Morogoro urefu wa kilometa 300 umefikia asilimia 47.87 kwa mujibu wa taarifa ya Machi, 2019.

Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye wakati akijibu swali la Mbunge wa Msalala(CCM), Ezekiel Maige.

Katika swali lake, Maige alisema Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 imeilekeza serikali kujenga upya reli hiyo na Rais tayari ameshapata fedha za mkopo kutoka serikali ya China kwa ajili ya utekelezaji huo.

“Je, utekelezaji wa ahadi hiyo ya CCM na Rais John Magufuli kwa mradi huu umefikia hatua gani? Na kwa kuwa Isaka ni eneo la makutano ya Reli ya Tabora-Mwanza na Reli mpya kati ya Isaka hadi Kenza na hatimaye Kigali-Rwanda, Je, serikali iko tayari kuifanya Isaka kuwa ndiyo karakana kuu?,”alihoji.

Pia alihoji serikali imejipangaje kuwasaidia wananchi waishio jirani na mradi huo ili wanufaike kiuchumi wakati wa ujenzi huo.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Nditiye alisema serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania(TRC) inaendelea na ujenzi wa reli hiyo kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ni kutoka Dar es salaam hadi Mwanza urefu wa kilometa 1,219.

Alifafanua kuwa ujenzi huo ni kutoka Tabora hadi Kigoma urefu wa kilometa 411, Kaliua- Mpanda hadi Karema kilometa 320, Isaka hadi Rusumo kilometa 393 na Uvinza kuelekea Musongati kilometa 150.

“Hivi sasa ujenzi wa awamu ya kwanza utekelezaji wake umefikia asilimia 47.87 na ujenzi wa kipande cha pili kutoka Morogoro hadi Makutupora kilometa 422 umefikia asilimia 7.96 kwa mujibu wa taarifa ya Machi, 2019,”alisema.

Aidha alisema Mpango wa serikali ni kuendelea kuifanya Isaka kuwa Bandari Kavu kwa ajili ya kuhudumia shehena itakayobebwa na reli ya sasa(Meter Gauge) na pia ya kisasa SGR.

“Aidha, kwenye mradi wa ukarabati wa reli iliyopo kupitia mkopo wa Benki ya Dunia itahusisha na ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhudumia shehena,”alisema.

Alisema uamuzi wa kujenga au kutojenga karakana kuu Isaka utafanywa wakati wa kufanya usanifu wa misingi kutoka Makutupora-Mwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *