Tisa wakamatwa kwa matukio ya ubakaji

Vyombo vya dola Mkoani Kigoma vinawashikilia vijana tisa wanaotuhumiwa kwa matukio ya ubakaji.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Wilaya ya Kigoma mjini, Samson Hanga alisema kuwa baada ya kuwepo taarifa hiyo ya vijana wanaoingilia akina mama kingono kwa nguvu, vyombo vya dola viliendesha zoezi la msako mkali kwa kushirikiana na wananchi ili kuweza kuwakamata wahalifu.

“Tulitengeneza namna namna bora ya kubaini wahusika kwa kushirikiana na wananchi, sababu hili jambo linafanyika kwa siri na wahanga wanatambua sura za watu hao na ni watu wanaoishi nao. Tulifanya zoezi la upigaji kura ya siri tukapata majina na majina mengine tulipata kupitia vyombo vya dola”

Alisema, mpaka sasa wamesha kamata vijana 9 wapo mahabusu na upelelezi dhidi yao bado unaendelea.

Alifafanua kuwa, kati ya waliopigiwa kura kuhusika na matukio ya ubakaji, kijana Hussein Hamisi maarufu kama Orosho ametajwa mara nyingi sana na kina mama waliofanyiwa ukatili na hivyo  anatuhumiwa kuwa kinara wa matukio ya hayo ya ubakaji.

“Orosho alipopata taarifa kuwa anatafutwa alikimbilia kwa mama yake kijiji cha Kagongo baadae akakimbia tena kijiji cha Kagunga lakini juzi jioni tulifanikiwa kumkamata Wilayani Kasulu na kumpelekwa kituo cha polisi kwaajili ya hatua zaidi,” alisema.

Kuhusu ukamataji, alisema, zoezi bado linaendelea kwani walipata listi kubwa ya majina kupitia  zoezi la upigaji kura lililoendeshwa na kuongeza kuwa, gwaride la utambuzi kwa waliokamatwa linaendelea.

Jina la teleza, lilitokana na kwamba, wakati wa usiku kuna wanaume walikuwa wakiingia kwenye nyumba wanazoishi wanawake na kuwabaka ambapo watu hao kabla ya kufika kwa mwanamke mlengwa huvua nguo zote na kubaki kama alivozaliwa, kisha wanajipaka grease ama mafuta ya kula mwili mzima. Baada ya hapo hubeba silaha aina ya kisu kikali ama mapanga, huvunja, ama hubomoa na kuingia kwenye nyumba anamoishi mwanamke kwa nia ya kubaka, kujeruhi, kuharibu mali na kuiba.

Taasisi ya Change Tanzania inabainisha kuwa, tatizo hilo limeanza tangu mwaka 2016, ambapo wanawake kadhaa walijeruhiwa na mmoja wa wanawake hao akaamua sasa lazima apaze sauti yake, ndipo wanawake wengi wakaanza kujitokeza juu ya suala hil0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *