Polepole:Wabunge wanaochonga mchakato wa manunuzi ya korosho hawataliona bunge la 2020

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, ameeleza kuna wabunge wa chama hicho ambao wamekuwa wakiikosa serikali kwa mema wanayoyafanya watakuwa na wakati mgumu mfikapo mwaka 2020 na kuwataka kutafuta kazi nyingine.

Polepole aliyasema hayo katika mahafali ya wanafunzi wa vyuo wa chama hicho mkoani Mtwara, huku akieleza korosho ni zao linaloteta fedha nyingi ingawa kuna mabeberu wanalitumia kama fimbo ya kuwachapa Watanzania.

Alisema kuna wabunge wenye nongwa kila serikali inapotatua matatizo mbalimbali, ikiwemo kununua korosho wanashiriki nongwa , hivyo wanapaswa kujipanga mapema.

“Itabidi wajipange kwa sababu mimi na wenzangu kuanzia sekretarieti, kamati kuu na Halmashauri Kuu tupo kitu kimoja tumeweka mikakati sawa kulinda utu na heshima ya wakulima,” alisema

Licha ya kwamba Polepole hakutaja majina ya baadhi ya wabunge wa CCM ambao wamekuwa wakikosoa utaratibu ulitotumika katika kununua korosho.

Miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa wakipigania sakata la korosho ni Nape Mnauye ambaye ni Mbunge wa jimbo la Mtama (CCM) kwa kutaka serikali iwapatie haki wakulima wa zao hilo.

Mei 29 mwaka huu sakata la korosho lilishika kasi bungeni huku wabunge watatu wakiikalia kooni serikali na kuitaka kutoa majibu yatakayowaridhisha juu ya mchakato mzima wa uuzaji wa zao hilo nchini.

Wabunge wengine waliochangia sakata hilo kwa kina ni John Mnyika (Chadema-Kibamba) na Joseph Selasini (Rombo-Chadema) wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya kilimo kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Nape akitoa maoni yake alitaka waliohusika kulihujumu zao hilo wawajibike wenyewe na wasipofanya hivyo atapeleka bungeni kusudio kuwataja mmojammoja.

Alisema wapo wakulima ambao korosho zao zimechukuliwa lakini hadi sasa hawajalipwa fedha zao na kuitaka serikali kupeleka bungeni Sheria ya Korosho ili waipitie upya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *