Idadi ya vifo yaongezeka ugonjwa wa Kipindupindu Dar

Licha ya serikali kufanya jitihada mbalimbali katika kupambana na ugonjwa wa kipindupindu idadi ya vifo imeongezeka na kufikia watatu na wagonjwa 40 wakiwa wamelazwa jijini Dar es Salaam.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imeandaa kambi tatu za kutibu wagonjwa hao katika hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala.

Akizungumzia hali ya ugonjwa huo, Mganga Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Yudas Ndugile,alieleza kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanatoka katika wilaya ya Temeke na Ilala ikiwa na watu wachache.

“Wagonjwa wengi wanatoka Buza, Keko, Mtoni Kijichi, Tandika, Chamazi, Kivule na Mtaa wa Azimio ambao wapo katika wilaya ya Temeke,”

Dk. Ndugile alitaja maeneo mengine kuwa ni Mchikichini, Kigogo, Kariakoo, Vingunguti na Ilala kwa upande wa wilaya ya Ilala.

Aidha, alisema tayari wameshachukua tahadhari katika maeneo mbalimbali ya jiji kama, maofisa wa afya kufanya ukaguzi wa mazingira katika kata na mitaa yote pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuepuka kuenea kwa ugonjwa huo.

Alisema wananchi wanaakiwa kuchukua tahadhari ya kutotiririsha majitaka, kuzingatia usafi wa mazingira, kunawa mikono, vyakula kupashwa moto, kuosha matunda na mboga mboga ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu.

Juzi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliagiza Halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam kutoa adhabu kali kwa wale ambao wanatiririsha maji machafu wakati wa mvua.

Waziri alisema idadi ya wagonjwa walowapokea ni 32 ambao wapo katika kambi zilizotengwa katika hospitali ya Amana, Mwananyamala na Temeke huku akieleza ugonjwa huo unasababishwa na uchafu, hivyo kila mmoja anatakiwa kuhakikisha anakuwa msafi na mikono inakuwa salama.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *