Mashahidi katika kesi ya vigogo wa TPDC washindwa kufika mahakamani

Kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayowakabili vigogo watano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ikiwemo Mkurugenzi Mtendaji, James Mataragio katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kusikilizwa kwa sababu mashahidi wameshindwa kufika.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Aneth Mavika alidai leo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Mavika alidai kuwa kwa bahati mbaya hawana mashahidi kwa sababu waliowategemea mmoja ni mgonjwa na mwengine amehamia mkoani Dodoma, hivyo aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusikilizwa.

Upande wa utetezi katika kesi hiyo walidai mahakamani hapo kuwa hawana pingamizi na hoja zilizotolewa na upande wa mashitaka.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 20, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa na kuutaka upande wa mashitaka kuhakikisha kuwa tarehe hiyo mashahidi wanakuwepo ili kesi iweze kuendelea.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kaimu Meneja wa uvumbuzi, George Seni, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Utawala, Wellington Hudson, Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu, Kelvin Komba na Edwin Riwa ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa mipango.

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa wametenda kosa hilo kati ya April 8, 2015 na June 3, 2016. Inadaiwa wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC kwa nafasi zao, wakati wakitimiza majukumu yao kwa makusudi walitumia madaraka vibaya.

Washtakiwa hao wanadaiwa walibadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa mwaka wa manunuzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha airborne gravity gradiometer survey ndani ya ziwa Tanganyika bila ya kupata kibali cha bodi ya wakurugenzi ya shirika.

Inadaiwa kitendo hicho kinakiuka kifungu cha 49 (2) cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyohalali ya Dola za Marekani 3,238,986.50 ambazo ni sawa na Sh bilioni 7.2 kwa Bell Geospace.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *