Serikali imesema kuku wa kizungu hawaongezi kitambi

Serikali imesema hakuna utafiti wa kisayansi unaonyesha kuku wa kizungu(Broilers) wanashida katika afya za binadamu ikiwemo kuongeza vitambi.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji, kwa niaba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Katika swali lake, Mbunge huyo alisema watu wanaotaka kupunguza mwili au vitambi wanakatazwa kula baadhi ya aina ya nyama na kushauriwa kula samaki na kuku.
“Lakini katika nyama za kuku kuna kuku kutoka nje ambao wanauzwa wana mapaja kama watu, hao kuku wa kizungu (Broilers), je, hawana uhusiano wa moja kwa moja kwenye kuongeza vitambi kuku hawa,”alihoji
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ulega alisema ulaji wa kuku wa kizungu na ulaji wa kuku kwa ujumla wana proteini ambayo huwa inatokana na wanyama na mimea.

 


Alibainisha kuwa hakuna utafiti wa kisayansi uliothibitisha kuwa kuku hao wana madhara kwa binadamu.
“Ulaji wa kupitiliza ndio utakaoweza kusababisha hayo matatizo lakini Broilers hawana shida yeyote, kinachowafanya wakue ni homoni ambazo kisayansi ni Vitamini, kwa hiyo sisi wana sayansi tunachokifanya vyakula vya Broilers tunaweka vitamins za kutosheleza kuhakikisha ukuaji wao unakuwa ni ukuaji wa haraka kulinganisha na kuku wa kienyeji,”alisema.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Geita Vijijini(CCM), Joseph Musukuma, alihoji serikali inatoa ushauri gani kwa wasio na vitambi wale vyakula gani kwa kuwa pamoja na matumizi ya vyakula vya wanga bado wapo kwenye maumbile hayo hayo.
Akijibu swali hilo, Ulega alimshauri Mbunge huyo kuwaona wataalam wa lishe ili kumpangia vyakula vitakavyoweza kumsaidia kupata kitambi.
Naye, Mbunge wa Mlalo(CCM) Rashid Shangazi alihoji serikali inaushauri gani kwa watanzania kula vyakula gani kuepukana na vitambi.
“Kwasasa kuna ongezeko la uzito uliopitiliza na hata kina mama wana vitambi, nini kifanyike ili tatizo hili lisiathiri watoto kuwa na ongezeko la uzito uliopitiliza,”alihoji.
Ulega akijibu swali hilo, alisema vyakula vyenye wanga vinapoliwa vikapitiliza vinaongeza protein mwilini.
Aliwataka kula ulaji wa kuzingatia mlo bora na kwamba protein bora zaidi ni inayotokana na mimea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *