Udahili wa wanafunzi wa kada ya afya wasitishwa

BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), limefungua udahili wa wanafunzi wa ngazi ya astashahada na shahada huku likisitisha udahili wa wanafunzi wa kada ya huduma ya afya ngazi ya jamii kwa mwaka wa masomo 2019/20.

Hatua hiyo, imetokana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kulielekeza baraza hilo kuwa kwa mwaka huu hakutakuwa na udahili wa wanafunzi wapya wa kada hiyo hadi hapo itakapotangazwa tena.

Akizungumza  na waandishi wa habari leo mkoani Dodoma Mkuu wa Kitengo cha Udahili NACTE, Twaha Twaha, alisema utaratibu uliopo mafunzo yote ya kada ya afya yanasimamiwa na Wizara hiyo hivyo wamepokea maelekezo hayo ya kusitisha udahili.

Awali, Mkurugenzi wa Uzingativu, Ufuatiliaji na Tathmini wa baraza hilo, Dk.Jofrey Oleke, alisema baraza hilo limefungua rasmi udahili wa wanafunzi wa ngazi ya astashahada na stashahada kwa kozi zote isipokuwa ualimu.

“Udahili umefunguliwa rasmi leo na utaendelea hadi Septemba 2, mwaka huu kwa Vyuo vyote vinavyotoa mafunzo katika ngazi hizo,”alisema.

Hata hivyo, alisema kwa waombaji wa kozi za afya katika vyuo vya serikali watatakiwa ama kuomba moja kwa moja kupitia vyuo ambavyo vitawasajili kupitia ‘Institutional panel’ ya chuo husika.

“Pia wanaweza kuomba kupitia tovuti ya NACTE na kwa waombaji wa program za afya kwenye vyuo visivyo vya serikali na waombaji wa program nyingine zote watatakiwa kuomba moja kwa moja kwenye vyuo husika,”alisema.

Alisema vyuo hivyo vitapokea maombi na kufanya uchaguzi wa wanafunzi wenye sifa na kisha kuwasilisha NACTE majina ya waliochaguliwa kwa ajili ya uhakiki kabla ya kuyatangaza.
Adha, alisema vyuo vinatakiwa kuzingatia utaratibu wa udahili kama ilivotolewa na Baraza katika mwaka wa masomo wa 2017/2018

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *